Shilole; kilichokupata feri ni sawa tu, kwa nini ulalamike?
Wengine wanamuita Shishi Baby. Huyu
anathibitisha kuwa mwanamke akiamua, inawezekana. Kwa sababu historia
yake inaonesha kuwa ni mpambanaji, akitokea kudhalilishwa kimapenzi
akiwa na umri mdogo, hadi kuja kuwa staa mkubwa.
Katika muziki, anafanya vizuri sana,
kwani kila kukicha, anaonesha kuendelea, akifanya aina ya muziki ambao
awali ulikuwa Mduara, lakini kwa sasa ameuongeza vionjo vinavyomfanya
kuwa kivutio cha aina yake stejini.
Ana kazi nyingi nzuri, tangu alipoanza
na wimbo wake wa Lawama, zikiwemo Dume Dada, Paka la Bar, Chuna Buzi,
Namchuka, Malele, Nyang’angany’a na sasa kibao kipya alichomshirikisha
Barnaba, Say My Name.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa binadamu
wote, nje ya sanaa, ana maisha binafsi yanayoendana na matukio ambayo
mengi yanachagizwa na ustaa wake. Kwa mfano juzikati, akiwa na washkaji
ndani ya pantoni kuelekea Kigamboni.
Akiwa ndani ya gari na kidogo akionekana
kuchangamka, alikataa kushuka garini kama utaratibu ulivyo. Gari
halitakiwi kupakiwa kwenye pantoni likiwa na abiria, anatakiwa dereva
tu, ili aweze kulidhibiti endapo kutatokea dharura yoyote.
Shishi Baby alikataa katakata kushuka,
akiwaambia walinzi kuwa yeye ni staa mkubwa, hivyo aachwe avuke akiwa
‘amejilalia’ zake garini, jambo ambalo halikukubaliwa, hivyo kuwafanya
walinzi hao kumshusha kwa nguvu na ‘kumpumzisha’ kwa muda ili
kiburudisho alichopata kipunguze makali.
Hili ndilo tatizo moja kubwa sana kwa
hawa mastaa wetu, hasa hawa wa dotcom. Wanaamini kujulikana kwao ndiyo
leseni ya kufanya wanavyotaka, bila kujali kuwa kuna sheria na taratibu
ambazo lazima zifuatwe, bila kujali ‘taito’ yako, iwe msanii,
mwanasiasa, mwanasheria au yeyote yule.
Na ubaya zaidi, hawafahamu kuwa wao
ndiyo wanastahili kuwa namba moja katika kuzifuata na kuzitii sheria na
taratibu hizo, ili wawe mifano kwa wengine, hasa mashabiki wao.
Inashangaza kuwa hawafahamu kwamba kuna
watu ukiwatajia Shilole wala hata hawaelewi unasema nini. Siyo kila mtu
anafuatilia muziki, filamu au chochote unachokifanya. Sasa unapoingia
kwenye kazi ya mtu na kusema eti; ‘kwani hunijui mimi?’ unampa majaribu
tu ya bure. Kwani wewe nani katika nchi hii?
Unaweza kufika ofisi ya umma na
kujitambulisha, ukitegemea kila mtu anakufahamu, hapana. Kuna wengine
hawafuatilii kabisa Bongo Fleva, hawajui hata filamu za Kibongo zikoje,
sasa wakisema hawakujui usifikiri wanatania na hata kama wanakujua,
ndiyo uvunje sheria?
Nimshauri tu dada yangu Shilole, katika
kufuata sheria na taratibu, anapaswa kuwa mstari wa mbele ili
wanaomshabikia nao watambue kuwa wanapaswa kuzingatia, vinginevyo kama
unataka kuutumia ustaa, basi ni kwenye viwanja vya burudani ambako
wanaofika ni wale wanaokufahamu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni